Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Albert Chalamila amewataka Wakurugenzi kuacha kulalamika na kuilaumu Serikali kuwa imewanyang’anya mapato na badala yake wajikite katika kuibua vyanzo vipya vya mapato ili kuinua uchumi wa halmashauri.
Hayo ameyasema jana alipokuwa akihutubia katika baraza la Madiwani la kujadili hoja za Mkaguzi mkuu wa Serikali (CAG) za mwaka wa fedha 2017/2018 lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya Wilaya ya Busokelo.
Mhe. Chalamila amesema kuwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli ametoa vitambulisho vya wajasiriamali ili kuwapunguzia kero za ushuru mbalimbali lakini wataalamu wanatakiwa kukaa chini na kubuni vyanzo vipya ambavyo havina makelele.
“Kuna baadhi ya Wakurugenzi ambao waliingia kwenye dimbwi la kulalamika..kwamba amenyang’anya mapato ya halmashauri yetu, nadhani huu si wakati wa kulalamikia masuala ya Kitaifa”. Alisema Mhe. Chalamila
Mhe. Chalamila aliongeza kuwa, jambo la muhimu ni kukusanya takwimu zaidi ili makadirio ya mapato yaendane na kinachokusanywa kwani inapoonekana kunakuwa na mpishano mkubwa basi ijulikane kuwa wataalamu hawakufanya kazi ya kutosha.
Mkutano huo umefanyika ikiwa ni sehemu kutoa majibu ya hoja za mkaguzi Mkuu wa Serikali za mwaka wa fedha 2017/2018 ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo imepata hati inayoridhisha ikiwa ni mwaka wa nne mfululizo.
Lwangwa, Tukuyu
Anuani ya Posta: S. L. P. 2, Tukuyu
Simu: +255 737 205 318
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@busokelodc.go.tz
Hakimiliki ©2019 Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo. Haki zote zimehifadhiwa.