1.0 Utangulizi.
Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo ina ukubwa wa eneo la hekta 96,914.0 (969.14 km2). Eneo lifaalo kwa kilimo ni hekta 49,389.67 na eneo linalolimwa kwa sasa ni hekta 41,176.7 sawa na asilimia 83.4 ya eneo linalofaa kwa Kilimo. Aidha Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo ina jumla ya kaya zinazojishughulisha na kilimo 24,133 zenye wastani wa wakulima 72,401.
Kanda za Kilimo:
Halmashauri ya Busokelo imegawanyika katika kanda kuu tatu za kilimo, ukanda wa Chini, Kati na Juu. Katika kanda hizo tatu zinatofuatia kwa tabia ya hali ya hewa na mazao yanayolimwa kama ifuatavyo;
Ukanda wa chini:
Unaundwa na Kata za Kisegese, Kambasegela, Ntaba, Itete, Lufilyo na sehemu ya kata ya Lupata katika vijiji vya Ntapisi na Bwibuka. Ukanda huu ni maarufu kwa uzalishaji wa mazao ya mpunga, mahindi, mihogo, maharage, mbaazi, kokoa na matunda mbalimbali. Pia wakulima wa maeneo haya hufuga ng’ombe wa kienyeji (asili), mbuzi, nguruwe nk. Zana zitumikazo katika ukanda huu ni jembe la kukokotwa na maksai kwa 90%, pawatila kwa 10% na kwa upande mwingine jembe la mkono hutumika kwa 100%.
Hali ya hewa:
Ukanda huu ni wa joto na mvua za wastani kati ya milimita 800 – 900 kwa mwaka na kipindi kirefu ni cha ukame hivyo kilimo cha umwagiliaji kimepewa umuhimu mkubwa.
Miundombinu ya umwagiliaji:
Halmashauri ya wilaya ya Busokelo ina jumla ya skimu za umwagiliaji 12 ambazo ziko katika hatua tofauti tofauti za uboreshaji kama ifuatavyo; skimu 4 zimeboreshwa. Kifunda (Kata ya Lufilyo), Kisegese na Kasyabone (Kata ya Kisegese) na Mbambo (Kata ya Kambasegela).
Skimu 2 uboreshaji unaendelea; Katelantaba (Kata ya Ntaba na K/segela) na Mbaka (Kata ya K/segela na Ntaba).
Skimu 3 zimefanyiwa upembuzi yakinifu; Ndola na Katungila (Kata ya Lufilyo) na Kilugu (Kata ya Itete). Skimu 3 bado hazijaanza kufanyiwa uboreshaji (mifereji ya asili inatumika). Skimu hizo ni; Lusungo, Mwabuke na Ipyana zote zipo kata ya Lufilyo.
Skimu zote zitachangia eneo la umwagiliaji lipatalo ha 2800 uboreshaji ukikamilika. Mpaka sasa eneo linalo mwagiliwa ni ha 1183 sawa na asilimia 42.25.
Ukanda wa kati:
Unaundwa na Kata za Lwangwa, Kabula na Sehemu Kata ya Lupata katika vijiji vya Lupata, Mpanda na Nsoso Ukanda huu kwa sehemu kubwa umefunikwa na mazao ya kudumu kama migomba, kahawa, chai, miwa nk. Pia mazao mbalimbali ya msimu hulimwa katika ukanda huu kama mahindi, maharage, karanga, viazi vitamu, viazi mviringo, mihogo, mboga, mbogamboga na matunda mbalimbali.
Wakulima wa maeneo haya hujishughulisha pia na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na wa kienyeji kwa kiasi kidogo, nguruwe, mbuzi wa maziwa nk. Jembe la mkono hutawala katika ukanda huu kwa 98.6% na sehemu iliyobaki, zana za kukokotwa na wanyama na matrekta.
Ukanda huu unaundwa na Kata za Mpombo, Isange, Kandete na Luteba. Ukanda huu ni maarufu kwa kilimo cha viazi mviringo, mahindi, njegere, mazao ya bustani, na matunda. Wakulima wa maeneo haya pia ni wafugaji wa ng’ombe wa maziwa, nguruwe, mbuzi, kuku nk. Zana za kilimo zitumikazo katika ukanda huu ni jembe la mkono 97% na matrekta 3%.
Lwangwa, Tukuyu
Anuani ya Posta: S. L. P. 2, Tukuyu
Simu: +255 737 205 318
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@busokelodc.go.tz
Hakimiliki ©2019 Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo. Haki zote zimehifadhiwa.