CMT – BUSOKELO YAKAGUA MIRADI YA MAENDELEO, YAAGIZA MIRADI YOTE IKAMILIKE IFIKAPO 20/01/2026.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo (Wilaya ya Rungwe), Bw. Raphael Mputa, ameongoza Timu ya Menejimenti ya Halmashauri (CMT) kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika kata tofauti za Busokelo kwa lengo la kuhakikisha inatekelezwa kwa ubora, kwa wakati na kwa thamani halisi ya fedha. Zoezi hili la ukaguzi wa miradi limefanyika leo tarehe 15 Januari 2026.
Katika ukaguzi huo, Bw. Mputa amesisitiza kuwa miradi yote ikamilike ifikapo tarehe 20 Januari 2026 kama ilivyoagizwa na Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Mhe. Jaffar Haniu, katika ziara iliyopita, ili wananchi waanze kunufaika mapema na huduma bora za elimu, uchumi na utawala bora. Aidha, Timu ya Menejimenti ya Halmashauri (CMT) imehimiza usimamizi wa karibu wa miradi, utunzaji wa nyaraka na uwajibikaji katika kila hatua ya utekelezaji.
Miradi hii inalenga kuboresha huduma za elimu kwa watoto, kuongeza fursa za ajira na kipato kwa wananchi, kuwawezesha wanawake na vijana kiuchumi pamoja na kuimarisha miundombinu ya utawala, hivyo kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo.
Miradi iliyotembelewa ni pamoja na ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na matundu sita ya vyoo katika Shule ya Msingi Manambano, unaotekelezwa kwa fedha za BOOST zenye thamani ya shilingi milioni 70.1, ujenzi wa majengo ya Shule Mpya ya Msingi Lusanje – Mkonodo Mmoja, unaotekelezwa kwa fedha za BOOST zenye thamani ya shilingi milioni 329.5.
Miradi mingine ni pamoja na ujenzi wa madarasa matatu na matundu sita ya vyoo katika Shule ya Msingi Kandete, unaotekelezwa kwa fedha za BOOST zenye thamani ya shilingi milioni 88, ujenzi wa Shule Mpya ya Elimu ya Awali na Msingi Mwakaleli, unaotekelezwa kwa fedha za BOOST zenye thamani ya shilingi milioni 329.5,
Mradi wa Kikundi cha Wanawake Amka wa ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, unaotekelezwa kwa mapato ya ndani ya Halmashauri yenye thamani ya shilingi milioni 5.
Aidha, mradi wa ukamilishaji wa Nyumba ya Mkurugenzi wa Halmashauri, unaotekelezwa kwa fedha za Serikali Kuu zenye thamani ya shilingi milioni 70, pamoja na ukamilishaji wa Jengo la Utawala, unaotekelezwa kwa fedha za Serikali Kuu zenye thamani ya shilingi bilioni 1.
Miradi hiyo inatekelezwa kwa ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na Wananchi, ambapo Serikali imetoa fedha kupitia miradi ya BOOST, Serikali Kuu na Mapato ya Ndani, huku wananchi wakichangia nguvu kazi, ulinzi wa miradi na ushirikiano wa kijamii ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora na maendeleo endelevu katika Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo.
Kwa ujumla, miradi yote iliyokaguliwa ina thamani ya shilingi 1,892,100,000, fedha ambazo zinaonesha dhamira ya dhati ya Serikali kwa kushirikiana na wananchi katika kuboresha elimu, uchumi na utawala bora kwa maendeleo ya Busokelo.













Lwangwa, Tukuyu
Anuani ya Posta: S. L. P. 2, Tukuyu
Simu: +255 737 205 318
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@busokelodc.go.tz
Hakimiliki ©2019 Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo. Haki zote zimehifadhiwa.