Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo umeingia makubalianao na Kampuni ya Ujenzi ya Mzinga kwa kusaini mkataba wa ujenzi wa jengo la utawala la Halmashauri ya Busokelo.
Makubaliano hayo yamefanyika jana katika ofisi za Halmashauri kwa kutia saini mkataba wenye thamani ya Shilingi bilioni 1.4 ikiwa ni awamu ya pili ya muendelezo wa ujenzi wa jengo hilo la ghorofa moja.
Akiongea wakati wa kutia saini makubaliano hayo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo Mhe. Anyosisye Njobelo alisema kuwa wanabusokelo wana matumaini makubwa sana makubaliano yanayofikiwa kwani wanategemea kuona sura mpya jengo hilo na watumishi wanatamani kutumia ofisi zilizopo katika majengo hayo.
Aliongeza kuwa tangu halmashauri ianzishwe watumishi wamekuwa wakipata tabu kwa kufanya kazi katika mazingira magumu kwa kukosa ofisi za kufanyia kazi na kubanana kwenye vyumba vichache vilivyopo hali inayoleta ugumu katika kutekeleza shughuli za utoaji huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa uendeshaji wa Kampuni ya Ujenzi ya Mzinga Mhandisi Karumuma, alisema kuwa wanafurahi kwa kuaminiwa na kupewa dhamana na Halmashauri ya Busokelo kwa kuwa wataweza kukata kiu ya Watumishi wa Busokelo kwa kutimiza matakwa ya mkataba huo na wanachohitaji kutoka kwao ni ushirikiano.
Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo ni miongoni mwa Mamlaka za Serikali za Mitaa zilizoanzishwa hivi karibuni na moja kati ya changamoto zilizopo ni ukosefu wa jengo la Utawala ambapo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2012 wamekuwa wakitumia majengo ya taasisi zingine ikiwa ni pamoja na Ofisi ya Mbunge wa jimbo la Busokelo, jengo la tarafa na jengo la makumbusho ya Wanyakyusa.
Lwangwa, Tukuyu
Anuani ya Posta: S. L. P. 2, Tukuyu
Simu: +255 737 205 318
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@busokelodc.go.tz
Hakimiliki ©2019 Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo. Haki zote zimehifadhiwa.