MHE.HANIU AZINDUA ZAHANATI MPYA YA KIJIJI CHA ITETE.
Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Mhe. Jaffar Haniu amezindua rasmi huduma za matibabu katika zahanati mpya ya Selya katika Kata ya Itete.
Uzinduzi huo umefanyika leo 27/06/2024 katika kijiji cha Selya Kata ya Itete Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo.
Akizungumza na Wananchi wa Itete mara baada ya kukagua miundombinu ya zahanati hiyo pamoja vifaa tiba vilivyopo katika zahanati hiyo mpya, Mhe.Haniu amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan inahakikisha Wananchi wake katika maeneo yote nchini wanapata huduma bora za matibabu katika maeneo yao ya karibu.
"Wito wangu kwenu, ninaomba tuitunze zahanati hii, hii ni ya kwetu ni nguvu zetu na ujenzi tulianza wenyewe na Serikali yetu ilituongezea fedha za ukamilishaji vifaa tiba pamoja na Wataalamu, Serikali ya Awamu ya Sita inahakikisha Wananchi wake wanapata huduma bora za matibabu katika maeneo ya karibu ili kuondoa adha ya kusafiri umbali mrefu wa kufuata huduma za matibabu" Alisema Mhe. Haniu.
Aidha Mhe.Haniu amewataka Wananchi wa Itete kuitunza miundombinu ya Zahanati hiyo ili idumu na akasisitiza kuendelezwe ushirikiano baina ya Wananchi na Wataalamu walipo katika zahanati hiyo.
Katika hatua nyingine Mhe. Haniu amemshukuru Mkurungenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo pamoja na Diwani wa Kata ya Itete na Wananchi wote kwa kushiriki kikamilifu katika usimamizi wa miradi na kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi .
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo Bi.Loema Peter ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutenga kiasi cha fedha shilingi Milioni 85 kwaajili ya Ukamilishaji wa Zahanati hiyo, pia ameishukuru Kamati ya Ujenzi, Wananchi wa Selya na Mheshimiwa Diwani wa Kata ya Itete kwa kushirikiana tangu hatua za awali hadi kukamilika kwa zahanati hiyo.
Diwani wa Kata ya Itete Mhe.Gwandege M.Mwakigemo, Ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwezesha upatikanaji wa huduma muhimu za jamii kwa Wanakijiji wa Selya.
Ujenzi wa zahanati mpya ya Selya umegharimu shilingi Milioni 85 kutoka Serikali kuu, shilingi milioni 22 ikiwa ni nguvu za Wananchi na shilingi milioni 3 kutoka mfuko wa Jimbo.
Lwangwa, Tukuyu
Anuani ya Posta: S. L. P. 2, Tukuyu
Simu: +255 737 205 318
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@busokelodc.go.tz
Hakimiliki ©2019 Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo. Haki zote zimehifadhiwa.